Hali ya upatikanaji wa dawa katika zahanati na hospitali za serikali
inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya kushindwa kwa vituo vya huduma za afya
kununua dawa Bohari la Dawa (MSD) kutokana na malimbikizo ya madeni.
Kufikia Septemba 2014 deni ambalo Bohari la Dawa linadai hospitali na
vituo vya serikali limekua na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 102.
Mwishoni mwa mwaka 2013 deni hilo lilikuwa shilingi bilioni 76.4.
Bohari la Dawa litashindwa kabisa kununa dawa kwa sababu ya deni kubwa
inalodiwa na makampuni yanayouza dawa kwenye bohari hilo.
Sera ya
serikali ni vituo vya afya vya serikali kuwapa matibabu bure kina mama
wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee, watu wenye magonjwa
sugu, watu wasiojiweza pamoja na watu wenye ulemavu. Kundi hili ni
asilimia 75 ya wagonjwa wanaoenda kutafuta huduma katika vituo vya afya
vya serikali.
Inasikitisha na inaonesha namna serikali ya CCM
isivyomjali mwananchi wa kawaida, Waziri wa Afya anapozitaka hospitali
kulipa madeni ya bohari la dawa kwa kutumia nusu ya fedha za uchangiaji
zinazolipwa na wananchi. Hii ni sawa na kuzieleza hospitali hizo zisitoe
huduma bila malipo kwani robo tatu ya wagonjwa wake ni wale ambao
serikali imeeleza wape huduma bila malipo. Serikali imewafungia ngulai
kina mama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee, watu wenye
magonjwa sugu, watu wasiojiweza pamoja na watu wenye ulemavu kwa
kuwaeleza kuwa watatibiwa bure. Wengi wao hawapati huduma bila malipo.
Vyombo vya habari vimemnukuu Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mh.
Mwigulu Nchemba akisema kuwa kiasi cha fedha zilizotolewa kwa ajili ya
dawa katika mwaka 2013/14 ilikuwa shilingi bilioni 47 lakini ni shilingi
bilioni 7 tu ndizo zilitumika katika kununua dawa. Hata hivyo serikali
imeshindwa kueleza kwa nini kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha hizi.
Shilingi bilioni 40 zimekwenda wapi?
Wakati wananchi wa kawaida
wanakufa kwa kukosa dawa, serikali imeendelea kutumia mabilioni ya fedha
kuchakachua maoni ya wananchi katika Bunge Maalum la Katiba. Ikulu
imepanga kutumia bilioni 2.5 kuipigia kampeni Katiba Inayopendekezwa
kupitia vyombo vya habari. Rais anaendelea kutumia mabilioni ya shilingi
kufanya ziara zisizokwisha nchi za nje. Vigogo wa serikali na CCM
wanaenda kutibiwa nje ya nchi. CCM haina huruma na mwananchi wa kawaida.
UFISADI WA IPTL UNATISHA
Wakati Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu, Serikali ya CCM
imewawekea fursa wapambe wake kujichotea fedha za umma kupitia fedha
zilizowekwa katika akaunti maalum ya Escrow kwenye Benki Kuu ya
Tanzania. Akaunti ya Tegeta Escrow ilianzishwa baada ya Shirika la kufua
na kusambaza umeme la Tanzania TANESCO kudai kuwa kampuni binafsi ya
kufua umeme ya IPTL imekuwa inaitapeli TANESCO kwa kuitoza Capacity
Charge kubwa kuliko makubaliano yaliyoko katika mkataba. Toka
imeanzishwa kampuni ya IPTL imekuwa mzigo mzito kwa TANESCO na watumiaji
umeme wa Tanzania kwa sababu ya kuilipa capacity charge kubwa na
mashine zake zinatumia mafuta mazito kufua umeme. Mafuta mazito yana bei
kubwa zaidi ya mara mbili ya gharama za gesi.
Kama viongozi wa
serikali na TANESCO wangekuwa makini ingewezekana kabisa mitambo ya IPTL
kuwa mali ya TANESCO mwaka huu wa 2014 kwani mkataba kati ya TANESCO na
IPTL wa mwaka 1994 ulikuwa wa miaka 20 na baada ya hapo mitambo hiyo
iwe mali ya TANESCO. Isitoshe kampuni ya Mechmar Corporation ya Malaysia
ambayo ndiyo iliyoanzisha IPTL ilifilisika mwaka 2008. Kwa kuwa
kulikuwa na madai ya Mechmar na IPTL kuidanganya TANESCO na kampuni hiyo
kuwa imefilisika viongozi wa serikali na wanasheria wazalendo wangeweza
kujikwamua kutoka jinamizi na gharama kubwa za IPTL.
Badala yake
viongozi wa serikaliambao hawana hata chembe ya uzalendo kwa
kushirikiana na matapeli wakaamua kuchota dola milioni 122 za Escrow
Account na kuzikabidhi kwa kampuni ya kitapeli iliyodai kuinunua IPTL.
Kampuni ya VIP Engineering and Management iliyokuwa mbia wa Mechmar
Corporation ambayo haikuwekeza hata senti moja imelipwa dola milioni 70.
James Rugemalira mmiliki wa VIP Engineering and Management amekaririwa
kuyaita malipo hayo ni “vijipesa vya ugoro.”
Mwanasheria Mkuu wa
serikali amenukuliwa akieleza kuwa fedha hizo siyo za umma wakati
taarifa ya fedha ya TANESCO inaonesha kuwa ni fedha za akiba (Reserve
Funds). Inaaminika kuwa kuna fedha nyingine - dola milioni 128 katika
Tegeta Escrow Account ambazo zitachukuliwa na kampuni ya kitapeli
iliyonunua IPTL.
Viongozi wa serikali kushiriki kuihujumu TANESCO
kunaonesha jinsi CCM kimekuwa Chama Cha Mafisadi kisichokuwa na hata
chembe ndogo ya uzalendo.
Tunaisubiri kwa hamu taarifa ya ukaguzi ya
CAG ya Tegeta Escrow Account. Ni matumaini yetu CAG ameifanya kazi hii
kwa uadilifu na weledi wa juu bila woga na ataeleza ukweli wa ufisadi
huu. Waliofisidi na walioruhusu TANESCO iibiwe wawajibike na wachukuliwe
hatua za kisheria.
CHANGAMOTO KWA SERIKALI IJAYO YA UKAWA
Serikali ijayo itakuwa na changamoto kubwa. Pamoja na kutokuwepo Katiba
ya Wananchi, itarithi serikali yenye malimbikizo makubwa ya madeni ya
nje na ndani, matumizi mabaya ya fedha za umma na ukosefu mkubwa wa
uadilifu na uwajibikaji. Pamoja na kuainisha sera zetu, wataalam wetu
wanapitia kwa umakini uchambuzi wa matumizi ya fedha za umma, Public
Expenditure Review na taarifa za CAG kubaini vizuri maeneo muhimu ya
kusimamia ili kuokoa fedha za umma zinazotumiwa vibaya na kuziweka
katika maeneo muhimu ya kuwapa wananchi huduma bora za afya, kuboresha
elimu kwa watoto na vijana wetu, kujenga miundombinu imara, kuimarisha
kilimo na kukuza uchumi unaoongeza ajira. Kwa miaka 10 ijayo Tanzania
inaweza kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 10 unao ingeza ajira kwa
wingi kwa vijana wetu. Haya yanawezekana ikiwa tutakuwa na uzalendo wa
dhati na kuweka mbele maslahi ya wananchi wa kawaida na kutumia
raslimali na maliasili ya nchi kuleta neema kwa wananchi wote.
HAKI SAWA KWA WOTE
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti,
Jumapili, 09 Novemba 2014.